Monday, August 28, 2006

NASUBIRI MASWALI

Kama ambavyo tunatambua na nilivyowahi kudokeza mwanzoni mwa blog hii,mapenzi ni sanaa ndefu na pana sana.Nikijidanganya kwamba kila siku ya mungu nitakuwa naandika jambo moja au mawili kuhusu sanaa hii kwa upana wake,nitakuwa natenda dhambi.

Badala yake ndio maana nikashauri kwamba mwendo wa maswali kwa majibu ndio unaofaa.Mnaonaje? Kimya changu,kwa maana hiyo basi,kinaashiria kwamba nasubiri maswali yenu,mapendekezo yenu,hoja zenu na ujuzi wenu.Tafadhalini ulizeni bila woga nami nitawajibu.Kumbukeni hakuna swali la kijinga,maswali yote ni muhimu na yanastahili majibu endapo tu,hayamkwazi mtu yeyote.

Tuesday, August 22, 2006

WANAWAKE NA PESA


Msomaji mmoja wa blog hii kuhusu mapenzi (hakupenda kuweka jina lake) amekuwa wa kwanza kuuliza swali.Nitaliweka swali lake kwa kutumia italics likifuatiwa na jibu langu. Nitakuwa najaribu kuyaweka majibu yangu kwa ufupi sana(not in details) ili kuokoa nafasi na pia muda wako. Hata hivyo,tunaweza kuwasiliana kwa email kama utahitaji details zaidi na pia michango,mawazo,maoni nk yanakaribishwa sehemu ya mbele ya maoni.

SWALI:Sasa mimi nauliza kwa nini wasichana wengi wanapenda wanaume wenye pesa hata kama wana uwezo wa kupata pesa pia.Kwa nini wasijiamini nao kama wanaume na kufikiria kuwa pesa siyo jambo la maana sana kama unampenda mwenzio?

JIBU:Swali hili lina historia ndefu sana na ya aina yake. Ni swali lenye umri mkubwa pengine kama ilivyo dunia yetu. Ni swali zuri sana. Mara nyingi limeulizwa kwamba hivi mwanamke anataka nini zaidi,pesa,ulinzi au mapenzi na mapenzi motomoto kitandani?(Wenzetu wazungu lugha yao inaweza kutenganisha dhana hizi mbili kirahisi zaidi;love or good sex) Kwa bahati mbaya hata wanawake wenyewe wamejikuta kila mara wakipambanua mambo yote haya kwa sababu kwanza wanaume wenye sifa zote hizo hapo juu kwa pamoja ni kama hawapo na dunia imebadilika na inaendelea kubadilika.

Kabla sijaendelea mbele naomba ieleweke kwamba sio kila mwanamke anaweka pesa mbele na sio kila mwanamke duniani bado anaamini kwamb a yeye ni mtu wa kupokea,kuhudumiwa na kutunzwa tu.. Hali ni tofauti baina ya sehemu na sehemu,nchi na nchi,bara na bara,tamaduni na tamaduni. Kwa mfano hapa ninapoishi tamaa ya wanawake kupenda na kuthamini pesa inazidi kupungua kadri siku zinavyokwenda. Siku hizi wanawake nao wapo mstari wa mbele kuchangia kwa njia zote zinazowezekana kuboresha maisha na kwa maana hii mapenzi.

Sifa zinaenda kwa wale wanawake wanaojulikana kama “feminists” ambao kwa namna moja au nyingine wanachojaribu kufanya ni kumkomboa mwanamke kutoka kwenye fikra za yeye kuwa chombo cha kupokea tu bila kushiriki kwenye kutafuta na kutoa.

Pamoja na juhudi za dhati za wanasaikolojia katika kubadili muelekeo wa fikra za wale wanawake wanaothamini pesa na kubakia wakidhani kwamba jukumu la kutoa pesa,kuchangia matumizi,kuthamini mapenzi zaidi haliwahusu,bado wapo wengi wenye msimamo tofauti.Wao bado wamegubikwa na utando wa historia,utando wa saikolojia na pia utando wa nafasi ya mwanaume dhidi ya mwanamke au dhidi ya jamii inayomzunguka.

Msimamo wao ndio muuliza swali wetu, anaouwekea msisitizo;kwamba kwanini hata wale walio na hali nzuri kifedha bado wanadhani sio jukumu lao kusaidia,kuchangia katika matumizi?

Sababu kubwa,kama nilivyoanza kuanisha hapo juu ni fikra. Kihistoria,tangu mwanzo wa dunia hii mwanaume amekuwa mtafutaji na mwanamke akabakia nyumbani kulea watoto,kutunza kaya na kuhakikisha kwamba familia inakuwa bora. Katika nchi zetu za kiafrika,kwa mfano,utaratibu ukawa binti akue,akishavunja ungo basi aoelewe akaanzishe familia yake.Wazo la yeye kuandaliwa kama mtafutaji halikuwepo kabisa. Kwa bahati mbaya dunia tunayoishi hivi leo inatoa nafasi kidogo sana kwa ustawi wa taratibu kama hizo.Lakini je,fikra au utaratibu huo umetokomea vichwani mwa watu,hususani wanawake wenyewe? Jibu rahisi ni kwamba bado fikra ile ya mapokeo ipo miongoni mwa wanawake wengi.

Sababu ya pili ni ya asili kimaumbile na kisaikolojia vile vile. Kimaumbile mwanaume ameumbwa awe mkakamavu zaidi,awe mlinzi wa mwanamke.Ingawa siku hizi mambo yanazidi kubadilika ambapo utaona wanawake wengi katika shughuli ambazo hapo zamani zilidhaniwa kuwa za wanaume peke yao,bado kwa kiwango kikubwa, hali imebakia kama ilivyokuwa enzi za Adam na Hawa. Sasa “protection” hii haishii kwenye ulinzi wa kimaumbile tu kwamba nyumba ikivamiwa mwanaume ndiye anategemewa zaidi kuongoza mapambano dhidi ya wavamizi,bali huenda pia hata kwenye financial protectionism ambapo bila kujali mwanaume ana kiasi gani cha fedha,bado anategemewa kuwa mtoaji.

Mwishoni nashauri pia tusisahau watu wanaoitwa “sugar mummies”. Hawa pia ni wanawake ambao msimamo wao ni tofauti kabisa na wanawake wengi ingawa motives zao ni tofauti na mara nyingi zinaeleweka.Pengine siku moja tutapata nafasi ya kuzungumzia saikolojia zao pia.

KIDOKEZO: Hivi unafahamu kwamba mfalme wa Morocco wa karne ya 16 (Moulay Ismail) alikuwa na watoto wanaokadiria kufikia 1,042?

Monday, August 21, 2006

TUZUNGUMZE MAPENZI!

Kila mtu anajua habari za mapenzi,hata wewe unayesoma habari hii unajua habari hizi. Mapenzi ni matunda matamu na pia ni matunda machungu.Sijui inategemea nini lakini nadhani ni kadri unavyoyapata,unavyoyala,na unavyojisikia wakati unaanza kula au unapomaliza.
Blog hii ni ya watu wazima,watu wanaojua nini maana ya mapenzi au wanaojaribu kujua zaidi.Nimeamua kuanzisha blogu hii kwa sababu najua ipo haja ya watu kuendelea kubadilishana mawazo juu ya mapenzi,ngono na mengineyo yanayohusiana na miili yetu,zikiwemo afya zetu.Si mnajua kwamba kitumbua siku hizi kimeingia mchanga ndugu zangu?

Kwa hiyo keti kitako tuanze kuyachambua masuala ya mapenzi. Kwa utaalamu wangu wa masuala haya nadhani nitakuwa tayari kujibu maswali yenu,hoja zenu nk kuhusiana na mapenzi,kujamiiana(ngono) na mengi mengineyo. Jisikie huru kunitumia email au kuuliza swali lako hapa hapa,nitakujibu. Lakini kwa kuanzisha hoja,hebu niambie,mapenzi ni nini kwa jinsi unavyoelewa wewe?Ni kwanini eti watu wanauana,wanafarakana,wanachinjana,nchi zinaingia kwenye vita kisa mapenzi? Je hayo yanabakia kuwa mapenzi au chuki? Kuna uhusiano gani kati ya mapenzi na wivu?Yupi ana nguvu kumshinda mwenzake?